Monday, 10 March 2014

YANGA YAFA KIUME

Wachezaji wa timu ya Yanga wakipasha kabla ya mechi kuanza.

YANGA wameonyesha juhudi za kutosha, lakini wakajikuta wakiondolewa kwa matuta kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly, jana usiku.
Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Emmanuel Okwi (wa tatu kutoka kushoto) akipambana na mchezaji wa Al Ahly katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baina ya timu hizo iliyochezwa kwenye uwanja wa Max mjini Alexandria, jana Jumapili.
Yanga inaendeleza rekodi yake ya kutowaondoa Waarabu kwenye michuano ya kimataifa.
Mshambuliaji Said Bahanuzi ndiye atakayejilaumu zaidi, kwani alikuwa anakwenda kupiga penalti ambayo ingewaondoa Al Ahly lakini akapiga nje.

Awali  katika penalti tano-tano, mbili za Yanga zilipanguliwa na mbili za Al Ahly pia zikapanguliwa na kipa Deogratius Munishi ‘Dida’, hivyo kuwa 3-3. Penalti mbili za Yanga zilizopanguliwa ni za Oscar Joshua na Mbuyu Twite.
                                          Baadhi ya watu waliohudhuria mechi ya Yanga na Al Ahly.
Katika mchezo huo wa jana, Yanga ilihitaji sare ya aina yoyote ili kutinga kwenye raundi ya 16 bora, lakini ilifungwa bao 1-0, ikabidi penalti zipigwe moja kwa moja kwa kuwa awali Yanga walishinda 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wiki moja iliyopita.

Hata hivyo, Yanga walionekana kuwazidi ujanja Waarabu hao ambao walianza mchezo kwa kasi lakini kosa la dakika ya 73 lilimpa nafasi Said Abdulwahed ambaye aliifungia timu yake bao muhimu.
Hata hivyo, Al Ahly walikuwa wakijiangusha mara kwa mara kila walipofika kwenye eneo la hatari wakitaka kupewa penalti lakini mwamuzi alionyesha kuitambua janja yao akawa ‘anawapotezea’.
Wakati mchezo ukiendelea, mashabiki wa Al Ahly walivamia nje ya uwanja na kuleta vurugu kubwa, ikabidi polisi wapambane nao kwa kurusha mabomu ya machozi.
Haikuwa kazi rahisi kuwadhibiti, lakini kwa kuwa polisi walikuwa wengi, walifanikiwa kuwatuliza kwa mabomu ya machozi.

Hata hivyo, tofauti na ilivyotangazwa kuwa hakutakuwa na mashabiki kwenye mchezo huo, kuna baadhi ya mashabiki waliingia uwanjani na kuishangilia kwa nguvu Al Ahly, wakisaidiana na askari waliokuwa uwanjani hapo.

Wachezaji wa Yanga walionekana kuwa safi kisaikolojia kwa muda wote waliokuwa uwanjani na hawakuonyesha kutishwa na vurugu hizo za nje.
Ulinzi

Kama ungeibukia ghafla kwenye Uwanja wa Max mjini hapa jana ambako Yanga ilikuwa inavaana na Al Ahly ya Misri, hakika hali ya ulinzi ambayo ungeiona ingekutisha.
Nje ya uwanja huo kulikuwa na vifaru zaidi ya 10, polisi zaidi ya 200 na wanajeshi kama 100 hivi, waliokuwa wakirandaranda na silaha nzito ili kuhakikisha usalama wa kutosha unakuwepo.
Karibu eneo zima la uwanja huo lilikuwa limejaa askari wa jeshi na wa polisi, kiasi kwamba hali hiyo iliwatisha hata mashabiki waliokuwa wanajaribu kujisogeza uwanjani.

Mechi hiyo ilitakiwa kuchezwa bila uwepo wa mashabiki kutokana na vurugu ambazo hutokea mara kwa mara uwanjani katika michezo mbalimbali ambayo huchezwa nchini hapa.
Uwanja wa Max ndiyo ambao hutumiwa na Klabu ya Haras el Hadood ambayo iliwahi kucheza na Simba hivi karibuni kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na kuwatoa Wekundu hao wa Msimbazi.
Katika mchezo wa jana, kiungo Haruna Niyonzima wa Yanga aliugua malaria ya ghafla hivyo hakuweza kucheza.

Kikosi cha Yanga kilichoanza mchezo huo hivi; Deogratius Munishi ‘Dida’, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani, Frank Domayo, Simon Msuva, Mrisho Ngassa, Didier Kavumbagu, Emmanuel Okwi na Hamis Kiiza.

No comments:

Post a Comment