Pembezoni mwa Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu Tanzania (Tec),
ujenzi unaendelea wa barabara na daraja la kuunganisha Mji wa Kigamboni
na Jiji la Dar es Salaam, eneo la Mkondo wa Kurasini. Ujenzi huo
unafanywa na kampuni mbili kutoka nchini China.
Kampuni hizo ni; China Railway Jiangchang (T) Ltd
na China Major Bridge, mradi ambao unatarajiwa kukamilika Januari 2015
ukigharimu dola 136 milioni za Marekani, fedha ambazo asilimia 60
zinatolewa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na kiwango
kingine kinalipwa na serikali.
Ujenzi huo unafanyika ikiwa ni sehemu ya
kuwaondolea kero ya Kivuko wakazi wapatao 679,291 sawa na asilimia 5.7
ya watu wote wa Dar es Salaam na idadi hiyo ni tofauti na mamia wengine
ambao wanaenda eneo hilo kila siku kwa ajili ya shughuli tofauti
zikiwamo za kiuchumi.
Eneo la Kigamboni ambalo limelengwa kuwa mji mpya
wa kisasa, lina utajiri mkubwa wa mazao mbalimbali ya chakula, biashara
kama vile mbogamboga, matunda, viazi vitamu, magimbi, nazi, korosho na
mazao ya baharini wakiwamo samaki, mapambo ya majumbani na bidhaa
nyingine.
Pia mji huo una hifadhi historia kwani maeneo ya
Mbwamaji, Puna, Kimbiji, Pembamnazi, Buyuni na kwingineko kuna mabaki ya
majengo ya kihistoria ambayo hata hivyo yanatoweka kutokana na utunzaji
na harakati za ujenzi wa nyumba za kisasa.
Pia eneo hilo linasifika kwa kuwa na fukwe zenye
mchanga wa kuvutia na mandhari nzuri za kupendeza hali ambayo inachangia
kuwavutia watalii na wageni wengine wanaotembelea eneo hilo ambalo pia
upande mwingine ina hazina kubwa ya jiwe la jasi ambalo hutumika
kutengenezea saruji.
Kulingana na mkandarasi ambaye ni mbunifu wa mradi
huo ambalo ni la kuning’inia (Cable-Stayed Bridge), lina urefu wa mita
680 na upana wa mita 27.5 na linatarajiwa kuwa mbadala wa Kivuko cha
Kigamboni ambacho kina pantoni za Mv Kigamboni na Magogoni.
Ujenzi huo unakaribia kukamilika, lakini hadi sasa
gharama za kulitumia daraja hilo kwa wananchi wa kawaida, wenye magari,
baiskeli, mikokoteni na vyombo vingine bado hazijainishwa. Suala hilo
linawaacha watu weni katika maswali mengi kuliko majibu.
Ingawa hakijatajwa kiwango kitakachokuwa kinatozwa
kama ada na ushuru mwingine, lakini bado kuna utata iwapo mradi huo
utakamilika kwa wakati kutokana na sababu nyingi ikiwa ni pamoja na
ukweli kuwa mradi umefikia zaidi ya asilimia 50 ya ujenzi wake, lakini
kuna utata iwapo ujenzi utakamilika kwa wakati.
Hali hiyo inatokana na ukweli kuwa hadi hivi sasa
serikali haijatoa kiasi chochote kati ya asilimia 40 ya fedha ambazo
wanatakiwa kuchangia ili kukamilisha mradi huo hali ambayo inadaiwa
kukwamisha upatikanaji wa fedha za fidia kwa baadhi ya watu ambao
wanaguswa na mradi.
Msimamizi wa mradi huo, Mhandisi Karimu Mataka wa
Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), anakiri serikali kutokutoa
fedha ambazo iliahidi hadi sasa, na hali hiyo imechangia mradi kushindwa
kukamilika Januari mwakani kama ilivyokadirwa na badala yake sasa
unatarajiwa kukamilika Juni mwakani.
John Ngoma maarufu kwa jina la Jitu,mkazi wa eneo
la Kijibweni ambaye eneo lake limechukuliwa kwa ajili ya kutoa nafasi ya
utekelezaji wa mradi huo anasema ni vizuri wakaelezwa kiasi cha fidia
watakachopewa kabla ya uthamini kufanywa jambo ambalo linapingwa na
mfumo mzima wa fidia.
CHANZO MWWANANCHI
CHANZO MWWANANCHI
No comments:
Post a Comment