Afrika itawakilishwa na waamuzi wa kati watatu kwenye fainali za
Kombe la Dunia zitakazofanyika Brazil kwa mujibu wa orodha ya waamuzi
25 iliyotolewa na Shirikisho la Soka Kimataifa (FIFA. Kila mwamuzi
ataongoza timu ya wasaidizi wawili na hivyo kufanya idadi ya waamuzi
wasaidizi kutoka Afrika kuwa nane kati ya 50.
Fainali za Kombe la Dunia 2014 zitafanyika nchini
Brazil kuanzia Juni 12 mpaka Julai 13 ikiwa ni mara ya pili kwa fainali
hizo kufanyika kwenye nchi hiyo kigogo katika soka duniani. Mara ya
kwanza fainali hizo zilifanyika Brazil mwaka 1950.
Waamuzi hao ni Doue Noumandiez kutoka Ivory Coast,
Papa Gassama (Gambia) na Djamel Haimoudi (Algeria) ambao wataongoza
timu ya waamuzi watatu kila mmoja kwenye fainali hizo, kwa mujibu wa
utaratibu wa FIFA.
Doue atachezesha mechi za fainali hizo pamoja na waamuzi wasaidizi kutoka Burundi, Songuifolo Yeo na Jean Claude Birumushahu.
Gassama ataunda timu itakayowajumuisha waamuzi
wasaidizi Evarist Menkouande kutoka Cameroon na Kabanda Felicien kutoka
Rwanda, wakati Haimoudi ataongoza waamuzi wasaidizi Abdelhak Etchiali wa
Algeria na Redouane Achik wa Morocco.
Mwamuzi wa akiba kutoka Afrika Kusini Daniel
Bennett na Neant Alioum kutoka Cameroon wanakamilisha orodha hiyo ya
waamuzi kutoka Afrika. Katika orodha hiyo pia wamo Djibril Camara
(Senegal) na Marwa Range (Kenya).
Afrika imeendelea kushikilia idadi yake ya waamuzi watatu wa kati kwenye fainali hizo.
Kwa mujibu wa orodha ya FIFA waamuzi wengine ni
Ravshan Irmatov kutoka Uzbekistan, Yuichi Nishimura (Japan), Nawaf
Shukralla (Bahrain), Benjamin Williams (Australia), Joel Aguilar (El
Salvador), Mark Geiger (Marekani), Marco Antonio Rodriguez (Mexico),
Enrique Osses (Chile), Nestor Pitana (Argentina), Sandro Ricci (Brazil),
Wilmar Roldan (Colombia), Carlos Vera (Ecuador), Peter O’Leary (New
Zealand), Felix Brych (Ujerumani), Cuneyt Cakir (Uturuki), Jonas
Eriksson (Sweden), Bjorn Kuipers (Uholanzi), Milorad Mazic (Serbia),
Pedro Proenca (Ureno), Nicola Rizzoli (Italia), Carlos Velasco
(Hispania) na Howard Webb (England).
Mbali na Afrika, bara la Ulaya litatoa waamuzi
tisa, Shirikisho la Soka la Amerika ya Kusini (CONMEBOL) litatoa waamuzi
watano, huku waamuzi wanne wakitoka Asia (AFC), watatu kutoka
Shirikisho la Soka la vyama vya Amerika ya Kaskazini na Visiwa vya
Carribea (CONCACAF) na mmoja kutoka Oceania.
Akizungumzia uteuzi wa waamuzi hao 25, Katibu Mkuu
wa Fifa, Jerome Valcke alisema: “Waamuzi hao walichaguliwa kutokana na
uwezo wao, uelewa wao wa mchezo wa soka, uwezo wa kuusoma mchezo na
kuelewa timu zinazocheza zinatumia mbinu gani.”
Hata hivyo Valcke alisema kuna baadhi ya waamuzi
na wasaidizi wao wanaweza kuachwa Juni 12 wakati watakapowapima kwa mara
ya mwisho ili kujua kama wapo fiti kabla ya kuanza kwa mashindano.
Alisema: “Fifa ina utaratibu wa kuchagua waamuzi
bora ambao wapo fiti kwa ajili ya kuchezesha Fainali za Kombe la Dunia.
Huwa tunachagua waamuzi ambao wapo katika ubora wa juu kabla ya
mashindano.”
< mwananchi>
< mwananchi>
No comments:
Post a Comment