Katika hali ya kawaida mtu unapoamua kuwekeza au kufanya
biashara ya aina yoyote, suala la kupata faida au hasara ni lazima liwe
kichwani mwako. Jambo lingine ni la kuangalia ni kuhusu muda ambao
utatumika ili uwekezaji wako uanze kuleta tija pamoja na muda unaotumia
katika kusimamia biashara au uwekezaji wako.
Uwekezaji unapitia hatua mbalimbali kwani kuna
kipindi inawezekena soko lipo katika hali nzuri au mbaya. Endapo
ikatokea hali kuwa mbaya mwekezaji makini anapaswa awe na subira kwani
wakati mwingine hicho ni kipindi cha mpito.
Kwa wale ambao suala la subira halipo, siku zote
wanachukua uamuzi haraka kwa kuuza kitega uchumi husika na kupoteza
fursa ya kupata faida zaidi. Ili uwe mwekezaji mzuri unapaswa uwe
mvumilivu. Uvumilivu unategemea na kipato au umri kwa mfano, uvumilivu
kati ya mtu ambaye ni kijana hutofautiana na mzee au mtu aliyepevuka
ujana.
Uzoefu unaonyesha kwamba mwekezaji anayekaribia
kustaafu, uwezo wa kuvumilia hasara huwa ni mdogo ukilinganisha na
mwekezaji ambaye ni kijana. Mwekezaji wa mwanzo anakuwa anaangalia kile
ambacho amekichuma kwa muda mrefu, hataki kukipoteza kwani uwezo wa
kukirudisha unakuwa mdogo au haupo-tofauti na mwekezaji ambaye ni kijana
kwani ana muda mrefu wa kuweza kufidia hasara ambayo anaweza kuipata
kupitia uwekezaji ambao ameufanya uwe ni kupitia masoko ya mitaji au
sehemu nyingine.
Kuna watu wengine wanasema uwekezaji kupitia
masoko ya mitaji, upatikanaji wa faida ni mdogo sana ukilinganisha na
aina nyingine ya biashara kwa mfano, ufugaji wa kuku, kufungua duka la
vifaa vya ujenzi, biashara ya magari na aina nyingine ya biashara ambazo
zinapatikana katika ulimwengu huu.
Katika makala haya nitatofautiana na watu wenye
mawazo kama hayo hapo juu. Uwekezaji kupitia masoko ya mitaji una nafuu
ingawa faida inayopatikana siyo kubwa sana, pia ikumbukwe kuwa siku zote
uwekezaji wenye kutoa faida ya wastani ni endelevu.
Unafuu mwingine ambao ninauzungumzia ni katika
suala zima la kupoteza mtaji wote, katika aina hii ya uwekezaji suala
kama hilo linakuwa halipo kwani kuna kampuni ambazo hazifanyi vizuri
sokoni, lakini wale ambao waliwekeza katika hizi kampuni hawajapoteza
fedha zao zote.
Kitu kama hiki hakipo katika biashara nyingine
kama vile ufugaji kuku, kwani katika aina hii ya biashara unaweza kuwa
umeingia gharama kubwa za kukuza kuku hao, ghafla ugonjwa ukawakumba na
wote wakafa, moja kwa moja utakuwa umepoteza mtaji wako wote. Wakati
mwingine unakuta mtu amestaafu ndiyo anaanza kufanya biashara kwa
kutumia fedha alizolipwa wakati wa kustaafu bila hata kufanya utafiti
namna ya biashara ilivyo kisa ameona fulani anafanya na kusikia maneno
kuwa biashara fulani inalipa sana na yeye anaingia kichwa kichwa.
Ili mtu afanikiwe anapaswa uwe na uzoefu na
biashara unayotaka kufanya, katika ili wengi wao wanapokimbilia kununua
magari ya abiria na baada ya muda wanajikuta hawezi kutengeneza faida
ambayo walikuwa wanaitegemea awali, hapo ndiyo muda wa kufilisika na
kuanza kuishi maisha magumu kwani hakuna mshahara ambao utakuwa unaingia
zaidi ya kutegemea pesheni ambayo haiwezi kukidhi mahitaji yako yote.
Wale ambao wanakuwa wamewekeza kupitia masoko
mitaji na kampuni walilizowekeza wanakuwa katika hali nzuri ya kifedha
kwani wanakuwa na uhakika wa kupata au kuingiza fedha kwa kila baada ya
muda fulani iwe ni kwa mwaka au kila baada ya miezi sita kupitia gawio.
No comments:
Post a Comment