Dodoma. Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, juzi na jana
wamekuwa katika mtihani mgumu wa kufikia uamuzi wa pamoja kuhusu utaratibu wa
upigaji kura, kati ya kura ya wazi na kura ya siri.
Habari kutoka katika kikao cha ndani cha Chama Cha Mapinduzi (CCM), zilisema
kutokana na mvutano huo, mjumbe mmoja, Chritopher Ole Sendeka, alijikuta akilia
hadharani akitetea upigaji kura ya wazi.
Kikao hicho kilichofanyika juzi kati ya saa 2:00 na saa 5:30 usiku chini ya
uenyekiti wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kilishuhudia mabishano makali kati ya
wanaotaka kura ya siri dhidi ya wale wanaotaka kura ya wazi.
Habari hizo zilisema baada ya Pinda kufungua kikao hicho, alimkaribisha
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa CCM, Shamsi Vuai Nahodha, ili atoe mrejesho
wa kikao cha mashauriano.
Inaelezwa kuwa katika kikao hicho, Nahodha aliwaambia wajumbe kuwa kutokana
na mazingira yaliyopo ndani na nje ya Bunge kwa upande mmoja na wananchi kwa
upande mwingine, kura ya siri haiepukiki.
“Kilio cha Ole Sendeka kwenye party cocas kikao cha chama (party cocus) juzi
usiku kilitokana na kauli ya Nahodha kwamba kura ya siri haiepukiki,” alidokeza
mbunge mmoja wa CCM aliyehudhuria kikao hicho cha faragha.
Mbunge huyo alilidokeza gazeti hili kuwa ndani ya kikao kulikuwa na mabishano
makali baada ya kauli ya Nahodha, huku baadhi ya wabunge wakisema wananchi
wamechoshwa na msimamo wa CCM.
Ni kutokana na mabishano hayo ndipo Ole Sendeka aliposimama akipinga
mapendekezo yaliyotaka CCM kulegeza msimamo na kuridhia kura ya siri na wakati
alipokuwa akizungumza alipobubujikwa na machozi.
Huku akilia katika kikao hicho, inadaiwa Ole Sendeka akisema kwamba kukubali
kura ya siri ni kuitosa CCM na msimamo wake wa kutaka muundo wa Serikali
mbili.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho, zilidai kuwa Ole Sendeka alienda mbali
zaidi na kusema endapo Pinda ataridhia kura hiyo ya siri, basi yeye (Pinda) na
viongozi waandamizi wa CCM waliohudhuria watawajibishwa na CCM.
Kutokana na mtafaruku huo, kikao hicho kilishindwa kufikia mwafaka na
kuahirishwa hadi jana saa 5:00 asubuhi ambapo hoja ya ama kura ya siri au ya
wazi, iliendelea kuwagawa wabunge katika makundi mawili.
Wakati akifungua kikao cha jana, Pinda alisema kutokana na yaliyotokea katika
kikao chao cha juzi usiku na baada ya kutafakari kwa mapana yake, chama kimeamua
kibakie na msimamo wake wa kura ya wazi. chanzo mwananchi
No comments:
Post a Comment