Amissi Tambwe(kulia), Nurdin Chona (kulia) wakiwa wamefungwa bandeji kubwa kichwani.
‘MWAKA wa shetani’ yawezekana hilo ndilo neno ambalo mashabiki wa Simba wanaweza kulitamka msimu huu, kwani timu yao imeambulia pointi moja katika Uwanja wa Sokoine huku mshambuliaji wao hatari, Amissi Tambwe akiumia kwa kupasuka sehemu ya kichwani katika mechi dhidi ya Tanzania Prisons, jana.
Simba imeambulia suluhu katika mechi hiyo iliyokuwa na ushindani kwa timu zote ambapo matokeo hayo yanaifanya iendelee kubaki katika nafasi ya nne ikiwa na pointi 36, nyuma ya Yanga inayoshika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 38, lakini Simba ipo mbele kwa michezo minne.
Mchezo huo ulishuhudia Tambwe akipata jeraha hilo baada ya kugongana na beki wa Prisons, Nurdin Chona, ambaye muda mwingi alikuwa akizunguka na Tambwe uwanjani hapo, kiasi cha mshambuliaji huyo raia wa Burundi kushindwa kucheka na nyavu kama ilivyo kawaida yake.
Tukio hilo lilitokea kipindi cha pili wakati wa kugombea mpira langoni mwa Prisons ambapo wote walianguka lakini Tambwe ndiye aliyeonekana kuumia kwa kiwango cha juu na kuvuja damu nyingi.
Hali hiyo ilisababisha daktari wa Simba, Yasin Gembe kumpa matibabu nje ya uwanja kwa dakika kadhaa kisha kumuuliza kama anaweza kuendelea. Tambwe alikubali kuendelea.
Tambwe anaongoza kwa mabao katika ligi hiyo akiwa na mabao 19. Alirejeshwa uwanjani huku akiwa na bandeji kubwa kichwani ambayo muda wote ilionekana kuloa damu. CHANZO GLOBAL PUBLISHER
No comments:
Post a Comment