Serikali inapotaka kufanya shughuli za maendeleo inaweza kuamua
kuuza hatifungani (bond) kwa umma na wananchi watakaponunua hizo
hatifungani wanakuwa wamewekeza. Hivyo utakuwa ni wajibu wa Serikali
kuwalipa riba hawa wawekezaji katika hatifungani hizo.
Jiji au Halmashauri pia zinaweza kuuza hatifungani
katika kuendesha shughuli za maendeleo katika jiji au halmashauri
husika. Kwa mfano ujenzi wa madaraja, hospitali pamoja na ujenzi wa
shule.
Kampuni binafsi pia inapotaka kufanya shughuli za
maendeleo, inakopa fedha katika taasisi za fedha au kuuza hatifungani.
Endapo kampuni imeamua kuuza hatifungani inakuwa inakwepa gharama za
kukopa katika taasisi za fedha.
Hatifungani ni hati ya deni ambayo kampuni au
serikali huwalipa wawekezaji kwa makubaliano maalumu na riba kulipwa na
marejesho baada ya kuiva kwa hatifungani.
Mwekezaji ambaye amewekeza katika hatifungani
anakuwa ni mwanahati. Hatifungani za Serikali na za kampuni binafsi
zinauzwa na kununuliwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).
Kuna hatifungani za Kampuni binafsi mbalimbali
ambazo zimeorodheshwa katika Soko la DSE. Kati ya kampuni hizo ni
Tanzania Breweries Ltd, ALAF Ltd, Standard Chartered Bank Ltd, Promotion
of Rural Initiatives and Development Enterprises Ltd (PRIDE) pamoja na
Bank M. Kati ya kampuni hizo, ziko ambazo zinatoa riba mpaka asilimia
15.
Ili kampuni iweze kuuza hatifungani kwa umma
inatakiwa ipate kibali kutoka kwa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na
Dhamana. Katika hili hakuna tofauti na pale kampuni inapotaka kuuza hisa
kwa umma katika soko la awali.
Hapa utayarishaji wa waraka wa toleo unatakiwa uwe
umeandaliwa pia. Waraka wa toleo unakuwa umebeba vitu vingi. Moja ya
vitu hivyo ni jinsi gani fedha zitakazopatikana zitatumika, kiwango cha
chini cha kufanya uwekezaji pamoja na athari za uwekezaji (risk factor)
katika kampuni husika.
Mwekezaji mtarajiwa anapowekeza katika
hatifungani, iwe za serikali au kampuni binafsi, anapata riba. Katika
upande wa uwekezaji katika hatifungani za serikali, mwekezaji anakuwa na
asilimia kubwa ya kupata riba ila kwa upande wa kampuni binafsi
mwekezaji anatakiwa afanye uchunguzi kuhusu kampuni husika kwani
asipofanya uchunguzi anaweza akawekeza sehemu ambayo si salama.
Mwekezaji katika hatifungani za kampuni binafsi
anatakiwa ajue moja ya mambo kama mfumo wa mtaji wa kampuni, uongozi
uliopo katika madaraka, kampuni husika ipo katika sekta gani ya biashara
pamoja na usalama wa kulipwa riba.
Katika suala la usalama wa kulipwa riba, wakati
nipo chuoni walimu walikuwa wanatuambia kuwa unapowekeza katika
hatifungani za serikali ni vigumu kutopata riba au si rahisi kupoteza
fedha kutokana na kuwekeza katika hizo hatifungani.
Katika hali ya sasa mambo yamebadilika kwani hata
Serikali inaweza kuyumba kiuchumi. Mfano mzuri ni baada ya kutokea
mdororo wa uchumi duniani kwani nchi mbalimbali zilikumbwa na huo janga
hilo hata watu ambao walifanya uwekezaji waliathiriwa kwa kiwango
kikubwa. :{chanzo mwananchi}
No comments:
Post a Comment