Dar es Salaam. Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL),limepata
ndege nyingine aina ya CRJ-200 ya Canada yenye uwezo wa kubeba abiria 50, ikiwa
ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wake madhubuti wa kuimarisha huduma
zake.
Ujio wa ndege hiyo kwa ATCL, umechukuliwa kama chachu ya kutimiza azma yake
ya kuimarisha huduma zake ikiwa ni pamoja na kuongeza safari zake katika njia
wanazoruka kwa sasa, kuanzisha njia mpya, na kuwahakikishia wateja wake huduma
za uhakika.
Baada ya kuwasili kwa ndege hiyo na kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Julius Nyerere Dar es Salaam, juzi usiku, Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa ATCL,
Kapteni Milton Lazaro alisema kuwa, kuna matumaini makubwa ya Shirika la Ndege
la Tanzania kufanya vizuri katika utoaji wa huduma za usafiri wa anga,
ikizingatiwa kuwa shirika limekuwa na mkakati madhubuti wa upanuzi wa huduma
zake na utekelezaji wake umeanza.
“Ndege tuliyoipokea leo(juzi) hii, ni sehemu ya ndege tatu tulizopanga kuleta
mwaka huu. Ndege nyingine mbili zinatarajiwa kufika kati ya mwezi Aprili na Mei
mwaka huu. Kuongezeka kwa idadi ya ndege zetu kutatuwezesha sisi kufungua mipaka
kwa kuanzisha njia mpya na kuongeza safari nyingi zaidi katika maeneo tunayoenda
kwa sasa,” alisema Kapteni Lazaro.
Alisema ndege mbili zitakazoletwa nchini mwezi Mei, zinauwezo wa kubeba
abiria 78 na ni toleo jipya katika sekta ya usafiri wa anga, zitatumika katika
kusafirisha abiria ndani na nje ya nchi.
Kapteni Lazaro alisema, shirika lake lina mpango wa kuanzisha safari mpya
ikiwa ni pamoja na Tabora– Mpanda, Mbeya-Dar es Salaam na kuongeza idadi ya
safari za Mwanza-Dar es Salaam, Dar es Salaam-Comoros, Mtwara pamoja na
Kigoma.
“Kwa ongezeko hili la safari zetu, abiria wetu watafurahia safari za kila
siku za kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza.Tutakuwa tukienda mkoani Mbeya mara
nne kwa wiki. Wakati Moroni katika Visiwa vya Comoro tutakwenda mara nne pia,
tunategemea kuzindua safari ya Tabora– Mpanda hivi karibuni,”
alisema.
Aliongeza kuwa shirika hilo limeondoa baadhi ya adhabu wanazotozwa abiria
endapo wanashindwa kusafiri siku na muda kama walivyoomba na kusema hii
itawasaidia abiria wao kutoingia gharama za ziada endapo watakumbana na dharura
yoyote kabla ya safari.
Ofisa Mtendaji huyo alisema, upatikanaji wa ndege hiyo utaongeza idadi ya
abiria kati ya asilimia 30 mpaka 40, kutokana na kuwa huduma za shirika hilo
bado ni nzuri na viwango vya nauli ni vya kiushindani zaidi na zenye unafuu
ukilinganisha na mashirika mengine.
Kwa kutumia ndege yake aina ya Bombardier Dash-8, ATCL kwa sasa inasafiri
katika zaidi ya maeneo nane (8) nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na Mtwara,
Mwanza, Tabora, Kigoma, Dar es Salaam, Mbeya, Bujumbura na Moroni nchini Comoro.
No comments:
Post a Comment