Mwenyekiti wa muda wa Bunge la katiba,Pandu kificho.
Bunge Maalumu la Katiba limepitisha
kanuni ya kuwazuia waandishi wa habari kuingia katika vikao vya kamati
za chombo hicho, hatua ambayo inaelezwa ni kinyume na Katiba inayotoa
uhuru wa wananchi kupata habari.
Kanuni hiyo ilipitishwa jana baada ya malumbano
makali yaliyowagawa wajumbe wa bunge hilo, baadhi wakipinga kifungu
hicho kwa sababu kinavunja Katiba ya nchi inayotoa uhuru kwa waandishi
kukusanya na kusambaza habari na wengine wakiunga mkono kuwazuia.
Kanuni hiyo ilipitishwa kwa mbinde huku baadhi ya
wajumbe wakiendelea kushikilia msimamo wa kuikataa, hata baada ya
Mwenyekiti wa Muda wa bunge hilo, Pandu Ameir Kificho kuridhia kipite.
Wajumbe waliopinga kanuni hiyo ni Joshua Nasari, Moses Machali, Peter
Serukamba, Ezekiah Wenje na Maria Sarungi.
Baadhi ya wajumbe akiwamo Katibu Mtendaji wa
Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga walisimama kutaka
kuzungumza lakini hawakupata fursa hiyo.
Mjumbe aliyekuwa mwiba kwa Tasnia ya Habari ni, Dk
Harrison Mwakyembe ambaye aliwashawishi wajumbe kufunga mjadala huo ili
wasonge mbele kwa madai kuwa hata yeye pia ni mwanahabari. “Hakuna
upande usiotambua umuhimu wa vyombo vya habari katika mchakato huu...
Tunachotofautiana ni jinsi na namna
ya ushiriki wa vyombo vya habari,” alisema Dk
Mwakyembe. Alisema Taifa limeingia katika kipindi maalumu kama cha vita
na kwa msingi huo, kanuni zinabadilika kulingana na mazingira na kwamba
vyombo vya habari vinapaswa kulitambua hilo.
Hata hivyo, Kifungu cha 57 (3) katika kanuni hiyo
kilipita baada ya kufanyiwa marekebisho kuondoa maneno ‘mwenyekiti
anaweza kutoa taarifa’ badala yake, ikawa ‘ni lazima kutoa taarifa.’
Kanuni hiyo inampa mamlaka mwenyekiti wa kamati au
mjumbe yeyote kwa idhini yake, kutoa taarifa kwa vyombo vya habari
kuhusu mambo yaliyojitokeza kwenye kikao.
Mjadala wakwama
Mvutano juu ya kifungu hicho ulianza juzi jioni wakati baadhi ya wajumbe walipotofautiana.
Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kumshauri
Mwenyekiti, Mjumbe George Simbachawene alisema iwapo waandishi
wataruhusiwa wangeweza kutoa taarifa zisizochujwa ambazo zitawachanganya
wananchi.
Hata hivyo, Mjumbe wa bunge hilo, Ezekiah Oluoch
alisema kisheria kanuni hiyo ilikuwa inakwenda kinyume na Ibara ya 18 ya
Katiba ya nchi ambayo kimsingi, ndiyo sheria mama. Aliisoma ibara hiyo
akisema kama wajumbe wataruhusu kupitishwa kwa kifungu hicho, litakuwa
kosa kubwa la kuvunja katiba ya nchi
.chanzo mwananchi
.chanzo mwananchi
No comments:
Post a Comment