
Dar es Salaam. Ikiwa imepoteza matumaini ya kutwaa ubingwa msimu huu na kuziachia vita hiyo Azam FC na Yanga, klabu ya Simba wanakabiliwa na safari ngumu ya siku 30 watakapocheza mechi zake tano zilizosalia msimu huu.
Wekundu hao wa Msimbazi walioko katika nafasi ya
nne wakiwa na pointi 36, wataanza safari hiyo ngumu Jumapili kwenye
Uwanja wa Taifa kwa kuumana na Coastal Union inayokamata nafasi ya saba
ikiwa imejikusanyia pointi 26. Pamoja na kupata kipigo kikubwa kwa Azam
wiki iliyopita, Coastal huwa sumbufu inapokutana na klabu kubwa.
“Mechi na Coastal itakuwa ngumu,” alisema Zdravko
Logarusic. “Sihitaji kuizungumzia sana, lakini nategemea matokeo yoyote
kwa timu yangu, kuwakosa (Amisi) Tambwe, (Betram) Mombeki na Uhuru
(Selemani) ni pigo.”
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza, Coastal
Union, ambayo iliweka kambi Oman mwishoni mwa mwaka, ililazimishwa sare
ya bila kufungana mjini Tanga.
Pia, Simba itashuka kwenye Uwanja wa Taifa Machi
30 kukwaana na Azam FC ambayo inakamata usukani wa Ligi Kuu ikiwa na
pointi 44, pia haijapoteza mchezo hata mmoja mpaka sasa.
Azam inapigana kufa na kupona kutwaa ubingwa wa Bara kwa mara ya kwanza baada ya kuukaribia kwa misimu miwili.
Mechi nyingine ya Simba ni dhidi ya Kagera Sugar Aprili 4 kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Mchezo mwingine utakuwa dhidi ya Ashanti United
Aprili 13 kwenye Uwanja wa Taifa. Ashanti iko kwenye vita kali ya
kukwepa kushuka daraja na hivyo itaipa Simba wakati mgumu.
Simba italazimika kufanya kazi ya ziada katika
mchezo dhidi ya mpinzani wake wa jadi Yanga iliyoko nafasi ya pili ikiwa
na pointi 40, ambao utachezwa Aprili 19 kwenye Uwanja wa Taifa.
Ili iweze kuinyima Azam nafasi ya kutwaa ubingwa, Yanga inahitaji kushinda mechi zote zilizosalia na kuiombea Azam kuteleza.
-mwananchi-
-mwananchi-
No comments:
Post a Comment