Thursday, 6 March 2014

KAULI MBIU YA SIASA NI KILIMO HATIMAYE YAKUMBUKWA IRINGA

Mwaka 1972, Mwalimu Julius Nyerere akiwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alitangaza Azimio la Iringa lililokuwa na kauli mbiu ya ‘Siasa ni Kilimo.’
Ilikuwa ni baada ya kufafanua falsafa ya maendeleo kwamba ili tuendelee tuna hitaji vitu vinne – watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.
Tafsiri ya maneno haya ni kwamba nguvu kazi na ardhi ni muhimu katika maendeleo ya kilimo nchini.
Hadi sasa sekta ya kilimo inayokua kwa asilimia nne, imeajiri asilimia 75 ya Watanzania, wengi wao wakiwa ni wakulima wadogo.
Serikali katika awamu zake tatu zilizotangulia ilijitahidi kuhamasisha kilimo kwa kuwaandaa wataalamu na kutumia wanasiasa katika majukwaa yao ili kuhimiza kilimo ambacho mpaka sasa hakina mafanikio ya kuridhisha.
Hivi karibuni kulikuwa na maadhimisho ya mwaka wa kilimo kwa Afrika, uliofanikishwa na Jukwaa la Kilimo (Ansaf) naTaasisi ya One ya Afrika Kusini, uliofanyika Kijiji cha Kaning’ombe wilayani Iringa, Mkoa wa Iringa.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma aliyemwakilisha Makamu wa Rais, Dk. Gharib Bilal, alikutana na kuzungumza na wakulima.
Mkulima wa mfano
Mkulima Eusebio Mbangile alipewa nafasi ya kuonyesha shamba lake kwa Dk. Ishengoma hivyo kuwa mfano wa utekelezaji wa Azimio la Siasa ni Kilimo.
Baada ya kusota na kilimo kisichokuwa na tija kwa muda mrefu, Mbangile ameibukia kuwa mkulima mwenye mafanikio baada ya kufuata ushauri wa kitaalamu akiwa na shamba la ekari 46 ambalo amepanda mahindi na miche ya matunda.
Mbangile anasema shamba lake ameligawa katika vitalu vitatu na kitalu cha kwanza amepanda mahindi ambayo anatazamia kupata magunia 25 kwa ekari moja.
“Eneo hili la pili lina ukubwa ekari nane ambalo analima bila kuweka mbolea ya kukuzia. Natarajia kupata gunia 15 hadi 16 kwa ekari moja.Nikiweka tofauti ya eneo la kwanza na la pili, naona hapa mazao yanapungua,” anasema Mbangile. Eneo la tatu ambalo lina ekari 3.5, mkulima huyo ametumia Sh1.7 milioni kuandaa shamba hilo.{CHANZO MWANANCHI}

No comments:

Post a Comment