Iringa. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe ataongoza wabunge 40 wa chama hicho
kwenda kuongeza nguvu katika kampeni za lala salama za uchaguzi mdogo wa
Jimbo la Kalenga, mkoani Iringa.
Uchaguzi mdogo wa Kalenga unatarajiwa kufanyika
Jumapili ijayo, Machi 16 mwaka huu kutokana na kifo cha aliyekuwa mbunge
wake, Dk William Mgimwa, huku mchuano mkali ukionekana kuwa kati ya
Chadema na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Habari ambazo zililifikia gazeti hili na
kuthibitishwa na Mbowe jana zinasema, wabunge hao watatawanywa katika
kata za Jimbo la Kalenga na watakuwa katika maeneo hayo hadi Jumapili.
Akizungumza kutoka mjini Dodoma, Mbowe
alithibitisha kwamba ataongoza wabunge 40 wa chama chake kwenda Kalenga
ili kuhakikisha chama hicho kinashinda uchaguzi huo mdogo.
Hata hivyo, Mbowe alisema safari hiyo itazingatia ratiba ya Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea Dodoma.
“Kama mnavyofahamu tupo hapa Dodoma ambako tuna
jukumu la kitaifa, kwa hiyo hatuwezi kuondoka tukaacha jukumu hili,
tunaangalia jinsi ratiba ilivyokaa ili pale tutakapopata fursa hiyo
tuweze kuitumia kwenda Kalenga,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Tunafahamu kwamba baada ya kupitisha Kanuni za
Bunge Maalumu, kuna kazi kubwa ya kuwaapisha wabunge, inaweza kuchukua
siku mbili au tatu hivi, kwa hiyo sisi tutatumia siku hizo kwa wabunge
wetu kwenda kuhakikisha ushindi unapatikana Kalenga.”
Alisema wabunge hao kabla ya kuondoka watashiriki
katika uchaguzi wa viongozi wakuu wa Bunge la Katiba; Mwenyekiti na
Makamu Mwenyekiti. Kwa mujibu wa ratiba ya shughuli za Bunge hilo,
uchaguzi wa viongozi hao unatarajiwa kufanyika leo na kesho.
Mapema Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa
Chadema, Benson Kigaila alisema baada ya kuwasili, wabunge hao watapiga
kambi katika jimbo hilo hadi uchaguzi utakapofanyika.
Tayari wabunge wawili wa chama hicho, Peter Msigwa
(Iringa Mjini) na Godbless Lema (Arusha) wapo Kalenga tangu Ijumaa
iliyopita wakimnadi mgombea wa Chadema, Grace Tendega. Ofisa Habari wa
Chadema, Tumain Makene alisema Mbowe anatarajiwa kuwasili leo Iringa
akitokea Dodoma.
“Mwenyekiti wetu anatarajia kuwasili mjini hapa
kesho (leo) akiwa na wabunge wengine 26, wanakuja kupiga kambi hadi
utakapofanyika uchaguzi Jumapili,” alisema Makene.
Katika hatua nyingine, Lema aliwatoa shaka
wananchi wa Kalenga kutokuwa na hofu kuhusu usalama wa kura
watakazozipiga, kwa kuwa chama hicho kimeimarisha ulinzi baada ya kura
kupigwa. Lema alisema Chadema kimewapeleka watu zaidi ya 1,000 ambao
wametawanywa vijijini na kwamba wengine kutoka Mara, Arusha na mikoa
mingine wanaendelea kuwasili kuungana na wenzao.
chanzo mwananchi
chanzo mwananchi
No comments:
Post a Comment