Abdulaziz Chende 'Dogo Janja' kutoka Ngarenaro.
ABDULAZIZ Chende ndilo jina lake halisi alilokuja
nalo jijini Dar es Salaam akitokea Ngarenaro, kule mjini Arusha, lakini
wajanja wa mjini wakambatiza kama Dogo Janja, ambalo kwa kweli limemkaa
vyema.
Ni bwana mdogo kweli, siyo tu kwa umri, bali hata sanaa aliyoichagua.
Ni kijana ambaye kwa jinsi watoto wa Dot.com walivyo, alistahili kuwa
kidato cha kwanza, pili au hata cha tatu. Ulimwengu wa Bongo Fleva,
ulimtambua baada ya kutambulishwa na Kundi la Tip Top Connection,
kupitia kwa kinara wake, Madee.
Dogo janja akiwa mzigoni.
Dogo anaweza kurap. Lafudhi yake ya watoto wa Kiarusha inamuongezea
‘credit’ katika muziki wake, kwa sababu nayo ni kitambulisho kingine cha
uwepo wake. Wakati akitambulishwa, Madee aliwaahidi mashabiki kuwa
atamlea Dogo katika njia inayofaa, ikiwa ni pamoja na kumkuza kisanii na
kielimu.
Simulizi zilisema alipelekwa Makongo Sekondari jijini Dar es Salaam.
Ghafla ukaibuka mzozo mkubwa baina ya Dogo na Madee, uliosababisha
Chalii kurudi zake Arusha. Sina sababu ya kurudia maneno yaliyoibuliwa
na pande zote mbili wakati ule kila mmoja akijisafisha mbele ya macho ya
watu.
Lakini kifupi Dogo Janja alilia kufanywa mgodi, akitumika
kumtengenezea hela Madee, kwamba alipiga shoo nyingi, lakini kipato
akawa hakioni, kinaishia kwa mkubwa. Na Madee naye alifunguka, akimlaumu
Dogo kwa kuzuzuka na jiji, kuacha shule na tabia nyingine mbaya.
Kwa sababu zilizo wazi, watu wengi walimuunga mkono Dogo Janja,
wakamsifu kwa kujitambua. Lakini bahati mbaya, baada ya kutoka Tip Top,
akadondokea Mtanashati Entertainments ambako baadaye taarifa zilisema
alifukuzwa kwa makosa yanayofanana na yale yaliyowahi kutolewa na Madee.
Habari ambazo bado hazijathibitishwa, zinasema kijana wetu amenyoosha
mikono, anataka kurejea tena Tip Top Connection, kule kule ambako ‘Rais
wa Manzese’ ndiye mfalme.
Kama nilivyosema pale awali, Dogo Janja bado ni kijana mdogo kwa
umri. Sanaa aliyochagua inahitaji mtu aliyetulia kichwani ili aweze
kufanikiwa. Kitu ambacho kingeweza kumsaidia kupata mwongozo bora katika
maisha yake, ni elimu pekee.
Ni jambo linalosikitisha kusikia kwamba anakimbia shule. Wakati flani
nilisikia alifeli sana katika mtihani wake, sababu kubwa ikiwa ni
kushindwa kuhudhuria vipindi darasani. Kama angetambua kuwa ujinga
alionao, ambao yeye anauona ujanja, ndiyo unaomfanya asiende shule,
hakika angetazama maili nyingi zaidi mbele na kujirudi.
Muziki wa Bongo umejaa dhuluma kila upande na watu hawa wabaya
wamejenga mtandao wa kulinda masilahi yao. Mtandao huu unawahusisha
watayarishaji wa muziki (producers), viongozi wa makundi, watangazaji wa
redio, maofisa masoko wa kampuni kubwa na hata wasambazaji wa kazi za
wasanii.
Msanii anatakiwa kuwa na kichwa kilichotulia kuweza kuushinda mtandao
huu. Ndiyo maana wasanii wakubwa kama AY na Mwana FA, licha ya ustaa
wao, walitumia sehemu ya mapato yao kurudi shule kujiweka sawa.
Msanii akikorofishana na mmoja kati ya wanamtandao, anaathirika sana.
Kwa sababu harekodiwi nyimbo nzuri, kazi yake haichezwi redioni na wala
hapewi nafasi ya kufanya shoo.
Kama angekuwa na elimu ya
kujitambua, angegundua kwamba wasanii wote, akiwemo Madee mwenyewe
wanaibiwa. Unafikiri hawa wanaoongoza makundi wana mapenzi gani na
wasanii wawasaidie kutoka, wao wakale wapi?
Na kusoma siyo lazima uwe na digrii, ni kiasi cha kujitambua tu. Ni
ile hali ya kujua kwamba kwa jinsi wingu lilivyo, inabidi utembee na
mwavuli kwani mvua inaweza kunyesha wakati wowote.
Dogo Janja bado hajachelewa, anao muda mzuri tu wa kuelimika, tena
kwa fedha zake mwenyewe. Ningekuwa mimi katika nafasi yake, nadhani
ningefanya maajabu, maana muziki ungenipatia elimu ambayo ingeboresha
maisha yangu kwa kiwango cha juu kabisa, umri na uwezo wake ni mtaji
ambao wengi wanautamani.
Kama amechagua kutembea katika njia hiyo, ambayo kwa bahati mbaya
kaka na dada zake nao wanapita, tusitarajie kuwepo kwa mabadiliko, siyo
tu ya muziki, bali hata wasanii wenyewe.
Kila siku tutawashuhudia wakiwasujudia watu ambao walipaswa kuwanyenyekea.
chanzo GPL