Dar es Salaam. Makosa ya mabeki
wa Simba yaliyofanywa dakika za majeruhi, yaliipa sare ya kwanza msimu
huu baada ya kufungana 2-2 na Coastal Union ya Tanga katika mechi ya
kupendeza iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana.Katika mchezo huo, Coastal walitumia dakika nane
za majeruhi kipindi cha pili kufunga bao la kusawazisha na kuinyima
Simba ushindi katika mechi yao ya kwanza msimu huu.Bao la Coastal lilitokana na makosa ya kiufundi ya
mabeki wa Simba walioshindwa kuweka ukuta imara kuzuia kiki ya adhabu
ndogo iliyopigwa na Ramadhan Salum dakika ya 82 na kwenda moja kwa moja
kwenye kamba za Wekundu hao.
Kosa la kwanza lililoigharimu Simba na kuipa
Coastal kupata bao la kwanza, lilifanywa na kiungo Pierre Kwizera
aliyeshindwa kuumiliki vizuri mpira kabla ya kunaswa na wachezaji wa
Coastal Union na Lutimba Yayo Kato kuutumbukiza wavuni kwa kiki ya
karibu na lango.
Kwa matokeo ya mchezo wa jana, Simba na Coastal Union zimezoa pointi moja kila mmoja.
Mchezo wa jana uliokamilisha mechi za kwanza za
raundi ya kwanza ya ligi hiyo, ulianza kwa Simba kusalimia lango la
wapinzani wao na kuandika bao la kwanza kupitia kwa Shaaban Kisiga.
Kisiga alifunga bao hilo kwa mpira wa faulo dakika ya saba kabla ya Amis
Tambwe kufumania nyavu dakika ya 36 akiunganisha kwa kichwa akimalizia
krosi ya Emmanuel Okwi.
Kwa upande mwingine, juhudi za Simba kupata mabao,
zilichangiwa kwa kiasi kikubwa na Okwi kwani bao la kwanza, aliangushwa
nje ya 18 na beki wa Coastal, Tumba Swedi kabla ya Kisiga kufunga kwa
faulo, pia alipiga krosi ambayo iliunganishwa na Tambwe kuandikia bao la
pili.Jitihada za Union kusaka bao zilizaa matunda katika dakika ya 67
baada ya Lutimba Yayo Kato kufanikiwa kumtungua kipa wa Simba, Ivo
Mapunda kufuatia pande la Itubu.
Ikishambulia mfululizo, Coastal Union ilisawazisha
dakika ya 82 kupitia kwa Ramadhan Salum aliyetandika mpira wa faulo
uliokwenda moja kwa moja nyavuni.
Simba waliianza mechi ya jana kwa kasi huku
wakitawala sehemu ya kiungo, lakini mipira yao ya mwisho haikuwa makini
na hivyo kushindwa kutengeneza nafasi za mabao huku Haruna Chanongo
akipoteza chache walizozipata.
Katika kipindi cha kwanza, Coastal walitumia muda
mwingi kulinda lango zaidi kuliko kushambulia, huku pia ikifanya
mashabulizi ya kushtukiza wakimtumia mshambuliaji Itubu Imbem.
Kipindi cha pili, Simba walifanya mabadiliko kwa
kuwatoa Chanongo na Tambwe na nafasi zao kuchukuliwa na Uhuru Selemani
na Rafael Kiongera, wakati Coastal waliwatoa Seleman Kibuta, Razak
Khalfan na Joseph Mahindi na nafasi zao kuchukuliwa na Lutimba Yayo
Kato, Ayoub Yahaya na Abbas Athuman.
Mabadiliko hayo yaliwanufaisha Coastal kwani
walipata mabao mawili. Akizungumza baada ya mechi kumalizika kocha wa
Simba, Patrick Phiri alisema: “Coastal walicheza vizuri, sijafurahia
matokeo tuliyoyapata ila tutajiandaa kwa ajili ya mechi ijayo.”
No comments:
Post a Comment