Monday, 8 September 2014

OKWI HURU KUCHEZA SIMBA

Wajumbe wa Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ya TFF wakiwa katika mkutano jijini Dar es Salaam jana. Picha na Said Khamis.      
Dar es Salaam. Utata wa Emmanuel Okwi umemalizwa rasmi na mchezaji huyo wa Uganda sasa yupo huru.
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ilikutana jana na kupitia masuala mbalimbali ikiwamo mgogoro wa kimkataba kati ya klabu ya Yanga na mchezaji Emmanuel Okwi.
Mkataba huo ulipitiwa na kamati ikiwamo kumsikiliza mchezaji mwenyewe pamoja na upande wa Yanga na kuridhika kuwa mkataba kati ya pande hizo umevunjika.
Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Boniface Wambura alisema jana kuwa mkataba wa pande mbili haupo kwa sababu Yanga ilikiuka kipengele namba 8 kuhusu malipo ya ada ya usajili.
“Yanga ikiwa mwajiri, haikutekeleza kipengele hicho cha kimkataba hadi kufikia Juni 27 mwaka huu ilipoandika barua TFF kuomba mkataba huo uvunjwe. Kwa maana hiyo Okwi ni mchezaji huru, hivyo yuko huru kujiunga na timu yoyote,” alisema Wambura.
Alifafanua kuwa mkataba ni uhusiano kati ya mwajiri (Yanga) na mwajiriwa (Okwi), ambapo Kamati imebaini kuwa uhusiano huo haupo, hivyo hakuna mazingira ya pande hizo mbili kuendelea kufanya kazi pamoja.
Pamoja na Yanga kuwasilisha pingamizi la kuwepo mmoja wa wajumbe katika kikao kwa sababu za kimaslahi (conflict of interests), walifahamishwa kuwa kilichopo mbele ya kamati ni mgogoro wa kimkataba kati ya Yanga na Okwi, na si usajili.
Pia lilijitokeza suala la Okwi kutakiwa na klabu ya Wadi Degla ya Misri.
Kamati imeiagiza Sekretarieti ya TFF kulifanyia uchunguzi suala hilo na kulitolea taarifa katika kikao kijacho.
Hata hivyo mjumbe ambaye Yanga ilimpinga hakushiriki katika kuchangia hoja na kutoa maamuzi.
Uamuzi wa kamati ulifanyika baada ya majadiliano, hivyo hakukuwa na suala la kupiga kura.
Kuhusu pingamizi la Coastal Union kwa Abdi Banda, Kamati imebaini kuwa klabu hiyo imevunja mkataba kati ya pande hizo mbili kwa kushindwa kumlipa mchezaji huyo mshahara wa miezi mitatu mfululizo kama takwa la mkataba.

No comments:

Post a Comment