
Moshi. Maofisa wa Polisi wapatao 120 wa Jeshi la Polisi, waliokuwa wakihudhuria mafunzo ya kupandishwa vyeo katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Moshi (MPA), wametimuliwa chuoni hapo.
Habari za uhakika zilizopatikana jana kutoka ndani
ya chuo hicho zamani kikijulikana kama CCP, zimedai uamuzi wa kuwaondoa
chuoni ulitangazwa jana na mkuu wa chuo hicho, Matanga Mbushi.
Vyanzo mbalimbali vililidokeza gazeti hili kuwa,
waliotimuliwa chuoni hapo ni maofisa ambao wana ulemavu wa aina
mbalimbali walioupata wakiwa wanatekeleza majukumu yao ya kazi.
Habari hizo zilisema hadi jana saa 9:00 alasiri,
maofisa hao walikuwa ofisi za mkuu wa chuo hicho wakisubiri kupatiwa
maelekezo ya namna ya kurejea katika vituo vyao vya kazi mikoa
mbalimbali.
“Wako 120 hivi walikuja hapa (MPA) kwa ajili ya
kuchukua kozi za Koplo, Sajenti, Meja na ‘Assistant Inspector’ (wakaguzi
wasaidizi), lakini ndiyo hivyo wametuambia tuondoke,” kilidokeza chanzo
chetu.
Hata hivyo, ofisa mmoja alilidokeza gazeti hili
kwamba mkuu wa zamani Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema, ambaye
amestaafu, ndiye wa kulaumiwa kwa kutoheshimu mapendekezo ya wataalamu.
“Tulimwambia IGP Mwema kwamba ni vizuri kama
maofisa wenye ulemavu kama baadhi ya vigezo wanavyo basi wapewe vyeo
huko huko mikoani, lakini wasiende chuoni,” alidokeza na kuongeza;
“Tulipendekeza yafunguliwe madarasa ya kanda
wakishafanya mtihani wa kawaida wapewe vyeo huko huko, lakini wakija
chuoni ni lazima wahudhurie vipindi vyote ambavyo vinafanya chuo kiitwe
chuo.
“Chuo chochote kile kina vigezo vyake na kwamba
ili mtu apate cheo alichokwenda kukisomea ni lazima ahudhurie asimilia
95 ya vipindi ikiwamo kwata, medani za kivita na kuzuia vurugu,”alisema.
Chanzo kingine kililidokeza gazeti hili kuwa
maofisa hao waliripoti chuoni hapo wiki mbili zilizopita na katika
uchunguzi, walibainika wana ulemavu ambao hawawezi kumudu mafunzo ya
ukakamavu.
Mmoja wa maofisa hao waliotimuliwa alilalamika
kuwa kitendo hicho siyo cha kiungwana kwa kuwa ulemavu huo waliupata
wakiwa kazini wakilitumikia Taifa na hawajashindwa kuingia darasani.
“Baadhi yetu tumefanya kazi miaka 20 wengine 25.
Wamekatika miguu. Wako trafiki wamegongwa na polisi wengine wamepigwa
risasi na majambazi wakapata ulemavu si sawa kutunyima vyeo,”
No comments:
Post a Comment