Wakazi wa Jiji la Arusha wakiwa katika Kituo cha Polisi mkoani humo
kushuhudia mwili wa mtu anayedaiwa kuwa jambazi sugu, Ramadhan Abdallah
Jumanne (Rama Ndonga), aliyeuawa kwa kupigwa risasi na polisi usiku wa
kuamkia jana. Picha na Happy Lazaro.
Mtu huyo aliyefahamika kwa kwa jina la Ramadhan
Abdallah Jumanne maarufu kama Rama Ndonga (37) Mkazi wa Moivo hatimaye
ameuawa polisi baada ya kupigwa risasi katika majibizano na askari wa
jeshi hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake
jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema jambazi
huyo aliuawa usiku wa kuamkia jana majira ya saa 2:04 usiku katika
Kijiji cha Moivo, Kitongoji cha Enaboishu wilayani Arumeru.
Alisema baadhi ya matukio ya ujambazi aliyowahi
kuhusika nayo ni lililotokea Agosti 6 mwaka huu saa 3:30 usiku maeneo ya
Kwa Iddi ambapo walimpiga risasi sehemu ya shingo mwanamke Shamimu
Rashid aliyekuwa Mkazi wa Sakini wakati akijiandaa kuingia nyumbani
kwake na kumuua.
Kamanda Sabas alitaja tukio lingine ni la Agosti
21 mwaka huu majira ya saa 1:00 huko maeneo ya Olasiti, jambazi huyo
akiwa na mwenzake kwenye pikipiki walimjeruhi kwa kumpiga risasi ya
mdomoni na kutokea kichwani mtoto Christen Nickson mwenye umri wa miaka
mitatu na nusu na kisha kufanikiwa kupora Sh200,000 na baadaye majeruhi
huyo alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Mount
Meru.
Aidha, kukamatwa kwa jambazi huyo ni baada ya
polisi kutumia mbinu za kisasa na kufika nyumbani kwa marehemu na polisi
walimwamuru ajisalimishe lakini alikaidi na kuanza kuwarushia risasi
hali iliyosababisha askari kujibu mapigo na hatimaye kusababisha kifo
chake.
Alisema kuwa, baada ya upekuzi mwili wa marehemu
ulipatikana na bastola aina ya Glock 19 yenye namba RLU 976
iliyotengenezwa nchini Australia ikiwa na magazine yenye risasi 14
ambayo alikuwa ameishika mkononi pamoja na maganda matano ya risasi.
Aidha, upekuzi zaidi uliofanywa katika chumba
chake ulibaini magazine moja yenye risasi 15 na magazine mbili zenye
uwezo wa kubeba risasi 30 kila moja, redio call moja yenye nembo ya
ITSS/UNICTR, pikipiki aina ya Toyo Power King rangi nyekundu yenye namba
za usajili T 507 BSU.
Upekuzi zaidi ulibaini kofia ngumu ya kuendesha
pikipiki rangi nyekundu, plate number ya pikipiki yenye namba T 805 CVD,
pingu moja, Glock Fab Defence moja na vifaa vya kusafishia bastola
pamoja na koti jeusi.
Kamanda Sabas alisema polisi wanaendelea kumsaka
mwenzake waliyekuwa wakitumia naye pikipiki hiyo, ili kuweza kuutokomeza
mtandao huo ambao umekuwa tishio jijini Arusha.
Kutokana na tukio hilo, watu walifurika kituo cha polisi kushuhudia mwili wa marehemu ambaye aliutikisa mji huo.
No comments:
Post a Comment